
Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF limetangaza
viingilio vya mchezo wa Jumamosi kati ya Tanzania dhidi ya Algeria utakaochezwa
katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam bei ya chini kuwa ni shilingi elfu
tano (5,000) tu.
Tiketi za mchezo huo zitaanzwa kuuzwa siku ya ijumaa
katika vituo mbalimbali vinavyotumiwa na TFF kuuzia tiketi, ambapo kiingilio
kingine kitakua ni elfu kumi (10,000) kwa viti vya VIP B & C, huku
kiingilio cha elfu tano kikiwa ni kwa viti vya rangi ya Bluu, Kijani na rangi ya
Machungwa.
Wakati huo huo kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania
‘Taifa Stars’ kinachodhamininiwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager,
kinatarajiwa kurejea nyumbani kesho Jumatano mchana kwa shirika la ndege la
Fastjet tayari kwa maandalizi ya mwisho ya mchezo dhidi ya Algeria siku ya
Jumamosi.
Stars iliyoweka kambi nchini Afrika Kusini imekua
ikifanya mazoezi kila siku katika uwanja wa Edenvale, ambapo mpaka sasa
wachezaji wote wapo katika hali nzuri hakuna majeruhi na kila mmoja yupo tayari
kwa mchezo wa Jumamosi.
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Charles Mkwasa amesema
vijana wake wapo vizuri kifaya, kifikra na morali ni ya hali juu “wachezaji
wamekua wakifanya mazoezi kwa nguvu na kuonyesha umakini mkubwa” alisema
Mkwasa.
Aidha Mkwasa amewaomba watanzania na wadau wote wa
mpira wa miguu nchini kujitokeza kwa wingi kuwapa sapoti ya kuwashangilia
vijana katika mchezo dhidi ya Algeria Jumamosi, kwani kutawafanya wachezaji
kujisikia wapo nyumbani na kucheza kwa nguvu zaidi.
Wachezaji wa kimataifa wa Tanzania Mbwana Samatta na
Thomas Ulimwengu walioshinda kombe la Ligi ya Mabingwa mwishoni mwa wiki na
klabu yao ya TP Mazembe wanatarajiwa kuungana na wenzao kambini kesho jijini
Dar es salaam.
Post a Comment