
Kamati
ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji iimeahirisha kikao chake kilichokuwa
kikae kesho Jumapili Septemba 4, 2016 kutoa hukumu ya shauri la mchezaji Hassan
Ramadhan Kessy anayedaiwa na Klabu ya Simba kuvunja mkataba kwa kuanza kufanya
mazoezi na klabu ya Young Africans sambamba na kusajili katika timu hiyo ya
Mtaa wa Jangwani, Dar es Salaam kabla ya mkataba wake kufika mwisho Juni 15,
2016.
Simba imelalamika mbele ya kamati
hiyo ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuwa, mchezaji Hassan Kessy
alivunja taratibu hizo akiwa ndani ya mkataba wa klabu hiyo yenye mashakani
yake Barabara ya Msimbazi jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamati
hiyo, shauri hilo lilisikilizwa baadaye mwezi huu katika tarehe itakayopangwa
hapo baadaye. Sababu za kuahirisha kikao hicho ni kutotimia kwa akidi ya
wajumbe wa kamati nzima. Akidi ni lazima wajumbe zaidi ya watatu wathibitishe
kushiriki.
Ilikuwa isikiliwe kesho baada
ya kushindikana kusikilizwa kwa shauri jingine linalohusu Klabu Simba
ikiilalamikia Klabu Young Africans, kuingia mkataba na mchezaji Hassan
Ramadhani Kessy wakati bado ana mkataba na klabu Simba.
Shauri la Simba dhidi ya Young
Africans lilishindika kusikilizwa kwa sababu Young Africans hawakutokea mbele
ya kamati hiyo wakati wa kusikiliza shauri hilo, hivyo kamati itaiandikia barua
Young Africans kukumbushwa kuhudhuria kwenye kesi hiyo Jumapili ijayo kabla ya
kutolewa uamuzi.
Kama hawakutokea tena, shauri hilo
litasikilizwa upande mmoja na kutolewa uamuzi upande mmoja. Kadhalika mashauri
mengine yatakayosikilizwa hapo baadaye ni pamoja na yale ambayo wahusika
walipewa nafasi ya kuyamaliza nje ya kamati lakini wakashindwa.
Post a Comment