
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF),
Jamal Malinzi kwa mara nyingine ametimiza ahadi yake kwa kuipeleka nje ya nchi
timu ya taifa ya Tanzania ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 ‘Serengeti
Boys’ ambako itapiga kambi ya utulivu kabla ya kucheza na Congo-Brazzaville
katika mechi ya mkondo wa kwanza kuwania nafasi ya kucheza fainali za Kombe la
Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri huo.
Benchi la ufundi lilimshauri Rais Malinzi kwamba
kambi hiyo ipigwe jijini Victoria, kwenye Kisiwa cha Mahe nchini Shelisheli.
Serengeti Boys inatarajiwa kuondoka nchini usiku wa kuamkia Jumatatu kwenda
Shelisheli ambako itafanya mazoezi maalumu kwa ajili ya mchezo huo ambao
utafanyika Septemba 18, 2016 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Hii ni mara ya pili kwa Malinzi kutimiza ahadi yake
kwa wachezaji hao. Kwa mara ya kwanza aliahidi kuwapa kambi ya nje kama
wangewatoa Shelisheli.
Timu kweli ilikwenda Madagascar kabla ya kuivaa
Afrika Kusini ‘Amajimbos’ na kuitoa na kwa sasa inakwenda Shelisheli kujipanga
kwa ajili ya kuitoa Congo-Brazzaville.
Serengeti Boys ambayo ilipiga kambi Hosteli za TFF,
zilizo Karume kwa siku nne kabla ya safari hiyo na Kocha Mkuu wa Serengeti
Boys, Bakari Shime maarufu kama Mchawi Mweusi amesema kwamba anaamini kuwa
mchezo ujao utakuwa mgumu kwa kuwa kila timu itajipanga kuvuka ili kucheza
fainali hizo.
Post a Comment