KATIKA kujiandaa vilivyo kuelekea mechi za raundi ya
pili ya Ligi Kuu soka Tanzania Bara (VPL), Klabu yasoka ya Azam FC, inatarajia
kukipima kikosi chake kwa kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Mtibwa Sugar
utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex, Jumamosi hii.
Azam FC iliyoanza maandalizi ya mzunguko huo wa pili
Jumatatu iliyopita, itautumia mchezo huo kuwapima wachezaji wake kabla ya
kuanza mikikimikiki ya ligi, ambapo inatarajia kufungua pazia kwa kucheza na
African Lyon Desemba 18 mwaka huu kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Baadhi ya wachezaji wapya itakaowatumia katika
mchezo huo ni washambuliaji Yahaya Mohammed (Aduana Stars) na Samuel Afful
(Sekondi Hasaacas), ambao wametua nchini wakitokea nchini kwao Ghana sambamba
na beki wa kati, Yakubu Mohammed (Aduana Stars) aliyekuja kufanya majaribio ya
kujiunga na Azam FC.
Mabingwa hao wanawafanyia majaribio wachezaji
wengine wawili kutoka Cameroon, beki wa kati Batetakang Flavius (Canon Yaoundé)
na kiungo mkabaji Stephane Kingue (Coton Sport FC de Garoua), ambao nao
wanatarajia kuwemo kwenye mtanange huo.
Mbali na kujiandaa na mzunguko wa pili wa ligi, Azam
FC pia inayatumia mazoezi hayo kujiandaa ipasavyo na michuano mingine ya Kombe
la Mapinduzi, Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) na Kombe la
Shiikisho Afrika (CC), ili iweze kufanya vizuri.
Post a Comment