Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu ya
Vijana wa Tanzania wenye umri wa chini ya miaka 15, imemaliza ziara Morogoro
kwa mafanikio baada ya jana Alhamsi Desemba 8, kuifunga Moro Kids mabao 3-1
katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Kwa siku ya jana Ijumaa Desemba 9,
mwaka huu timu hiyo ilijifua kwa mazoezi kwa mujibu wa programu ya Kocha Oscar
Mirambo baada ya Morogoro kuleta timu ya wakubwa tofauti na vijana wenye umri
wa chini ya miaka 15. Hivyo, mchezo huo wa pili haukufanyika.
Mazoezi na michezo hiyo ya kirafiki
ambayo mingine wataifanya Zanzibar juma lijalo, ni maandalizi ya mchezo wa
kirafiki wa kimataifa dhidi ya Burundi mchezo unaotarajiwa kufanyika Desemba
18, mwaka huu kwenye Azam ulioko Chamazi, Dar es Salaam.
Awali ilipangwa icheze na Shelisheli
ambayo imetoa taarifa ya kuwa haijajiandaa.
Mara baada ya Morogoro, timu hiyo
imerejea Dar es Salaam leo kujiandaa na safari ya kwenda Zanzibar Desemba 11
ambako itakuwa na michezo miwili mingine ya kirafiki.
Zanzibar itacheza na Kombaini ya
timu ya Vijana wa Zanzibar Desemba 12, 2016 kabla ya kurejea Bara Desemba 15,
kujiandaa na mchezo kirafiki wa kimataifa dhidi ya Shelisheli.
Kikosi hicho kinachonolewa na Kocha
Mkuu wa timu ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 14, Oscar Mirambo anayepata
ushauri kutoka kwa Mshauri Mkuu wa Maendeleo ya Soka la Vijana, Kim Poulsen.
Timu hii inaundwa na vijana ambao
TFF iliwakusanya tangu 2014 na kuwaunganisha kwa pamoja katika Shule ya Msingi
na Sekondari ya Kukuza Vipaji ya Alliance iliyoko Mwanza.
Timu hii inaandaliwa kuja kwa time
mpya ya Vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 ambao watashiriki fainali za
Kombe la Mataifa Afrika kwa vijana mwaka 2019 ambako Tanzania imeteuliwa na
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kuwa mwenyeji. Kambi itavunjwa
Desemba 18, mwaka huu.
Post a Comment